MASOMO YA MISA DOMINIKA YA 31 YA MWAKA "A" 5 NOVEMBA 2017

MWANZO:
Zab. 38:21-22
Wewe Bwana usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami, ufanye haraka kunisaidia, ee Bwana, wokovu wangu.


SOMO 1:Mal.1:14-2:8-10


Kwa maana mimi ni Mfalme mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu latisha katika Mataifa. Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi. Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema Bwana wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani Baraka zenu. Bali ninyi mmegeuka mkaiacha njia; mmewakwaza watu wengi katika sheria; mmeliharibu agano la Lawi, asema Bwana wa majeshi. Kwa sababu hiyo mimi nami nimewafanya ninyi kuwa kitu cha kudharauliwa, na unyonge, mbele ya watu wote, kama vile ninyi msivyozishika njia zangu, bali mmewapendelea watu katika sheria.
Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyeumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu?



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 131

(K) Ee Bwana, uilinde nafsi yangu katika amani yako.

Bwana, moyo wangu hauna kiburi,
Wala macho yangu hayainuki.
Wala sijishughulishi na mambo makuu,
Wala na mambo yashindayo nguvu zangu. (K)

Hakika nimeituliza nafsi yangu,
Na kuinyamazisha.
Kama mtoto aliyeachishwa,
Kifuani mwa mama yake,
Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu. (K)

Ee Israeli, umtumainie Bwana,
Tangu leo na hata milele. (K)


SOMO 2:1Thes.2:7-9,13


Kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe, vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu. Maaana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu. Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlilipokea lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.



INJILI
Yn. 6:63, 68

Aleluya, aleluya, 
Bwana maneno yako ni roho, tena ni uzima, wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 
Aleluya.


INJILI:Mt.23:1-12

Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupaua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza, atadhiliwa; na yeyote atakayejidhili, atakwezwa.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.
_____________

No comments:

Powered by Blogger.