MASOMO IJUMAA TAREHE 3 NOVEMBA 2017

SOMO 1:Rum.9:1-5


Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili; ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake; ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 147:12-15, 19-20 (K) 12

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)

Ndiye afanyaye Amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana. (K)

Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua.
Aleluya. (K)


SHANGILIO
Zab. 119:34

Aleluya, aleluya,
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya.


INJILI:Lk.14:1-6

Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponywa siku ya sabato, ama sivyo? Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato? Nao hawakuweza kujibu maneno haya.

No comments:

Powered by Blogger.