MASOMO YA MISA, FEBRUARI 1, 2018

ALHAMISI YA JUMA LA 4 LA MWAKA


SOMO 1
1 Falm. 2:1-4, 10-12


Siku ya kufa kwake Daudi ilikaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako; ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakenda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema) hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.
Basi Daudi akalala na babaze, akazikwa mjini mwa Daudi. Na siku alizotawala Daudi juu ya Israeli zilikuwa miaka arobaini; huko Hebraoni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu.
Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa imara sana.


Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Nya. 29:10-12 (K) 12


(K) Nawe watawala juu ya vyote, Ee Bwana.


Uhimidiwe, ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu milele na milele.

Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu,
Na kushinda, na enzi;
Maana vitu vyote vilivyo mbinguni
Na duniani ni vyako. (K)


Ufalme ni wako, Ee Bwana, nawe umetukuzwa,
U mkuu juu ya vitu vyote.
Utajiri na heshima hutoka kwako wewe. (K)


Nawe watawala juu ya vyote;
Na mkononi mwako mna uweza na nguvu;
Mkononi mwako mna kuwatukuza
Na kuwawezesha wote. (K)


SHANGILIO
Mk. 1:15


Aleluya, aleluya,
Ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili.
Aleluya.


INJILI
Mk. 6:7-13


Siku ile Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu, akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, Mahali popote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali popote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.


Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

No comments:

Powered by Blogger.