KUWENI WATU WA TOBA NA MSAMAHA-ASKOFU NZIGILWA
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa amewataka waamini wote kuyajongea maisha ya toba na msamaha na kufungua vifungo vya visasi kwa kumuomba Mungu awasimamie katika maisha hayo.
Askofu Nzigilwa ameyasema hayo katika mahubili kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa sakramenti ya kipaimara kwa vijana 120 wa parokia ya Mt. Karoli Lwanga iliyoko Yombo Dovya jijini Dar es Salaam.
“Kristo ametutangazia ya kuwa viwete wanaweza kutembea, vipofu wapate kuona na viziwi wapate kusikia kwa uponyaji kupitia mwanga wa msamaha. Nawaomba tujenge utamaduni wa kusameheana,” amesema.
Ameongeza kuwa, mtu akimuingia Kristo kwa uthabiti ni lazima ataona mabadiliko ndani ya nafsi yake.
Amewataka waimarishwa wa kipaimara wawe mabalozi wa upendo mahiri popote watakapo kwenda kwa kuiishi imani ya Kristo “Mkayatumie vizuri mapaji ya Roho Mtakatifu kwa kuiishi na kuishika imani, nanyi wazazi muwalee vizuri watoto hawa kwa kuwafundisha na kuwakumbusha yaliyo mema na kuwashirikisha kazi mbalimbali za Kanisa, ’’amesema Askofu Nzigilwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa parokia hiyo, Rosemary Kasongo amewaomba wazazi na wasimamizi wa watoto waimarishwa waendelee kuwa bega kwa bega na watoto ili wasipotee kwasababu mara nyingi watoto wanapokuwa wamepokea sakramenti hiyo hupotea ndani ya Kanisa na huonekana pale tu wanapohitaji kufunga ndoa.
Katika hatua nyingine waamini wa vigango vya Mbutu na Ngobanya katika Parokia ya Kimbiji jijini Dar es Salaam wameshindwa kujizuia kudondosha machozi baada ya Paroko Msaidizi wa parokia hiyo Padri Justus Lugayimkamu kuwaaga katika parokia hiyo ambapo mwezi huu anatarajia kuhamishwa na kupelekwa mahali atakapopangiwa kufanya utume.
Padri Lugayimkamu amehudumu kama Paroko Msaidizi parokiani Kimbiji kwa miaka mitatu na ushirikiano mzuri aliokuwa nao kwa waamini umewafanya watoe machozi.
No comments: