WAMISIONARI SIYO WAFANYABIASHARA NA ASKOFU DAMIAN DALLU
‘WAMISIONARI SIYO WAFANYABIASHARA' ASKOFU DAMIAN DALLU
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea Mhashamu Damian Dallu amesema kuwa wamisionari hawakuja nchini kama wawekezaji bali ujio wao ulilenga kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili, na ndiyo chanzo cha utoaji wa huduma za msingi za kijamii ikiwemo elimu, afya na maji.
Ameeleza hayo hivi karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu ya Upadri kwa aliyekuwa Shemasi Jerome Mponzi, katika Parokia ya Nyakipambo Jimbo Katoliki Iringa.
Askofu Dallu amesema kuwa wamisionari hawakujikita katika utoaji wa huduma za kiroho pekee, bali walihakikisha mwanadamu anakombolewa mzima mwili na roho, ndiyo maana walipojenga Kanisa walijenga pia vituo vya afya, hospitali au zahanati, shule na miradi ya maji.
“Sisi ndiyo tulioanzisha utoaji wa huduma za jamii kwa wananchi wote bila kubagua. Baada ya Serikali kuamka ndipo Mwalimu Nyerere akataifisha shule na miundombinu ya afya ili kuimarisha umoja wa kitaifa. Wazee wetu watangulizi walilielewa hili na hawakupiga kelele kwani waliona ni jambo jema linalowanufaisha watu wote. Baada ya muda huduma hizi zilizorota ndipo katika awamu ya pili baadhi yake zikarudishwa mikononi mwa Kanisa, na kisha Serikali kuingia mkataba ili wamisionari waendelee kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, kwa manufaa ya wengi, huku Serikali ikisaidia,” amesema.
Aidha Askofu Dallu ameongeza kuwa inashangaza kuona mtawa aliyekuja nchini mwaka 1950, akajitoa kuhudumia jamii bila faida, anafuatwa na kudaiwa kibali cha kufanya kazi nchini na kumtaka alipe kodi, na kusisitiza kuwa huku ni kumfanya mmisionari kuwa kama mfanyabiashara, jambo ambalo siyo sahihi.
“Sisi siyo dini ya mtu wala hatuna mwelekeo au msukumo wa kisiasa. Hatuhitaji upendeleo wa mtu bali tunafuata utaratibu uliowekwa. Tumesajiliwa chini ya Wizara inayohusika na Katiba na Sheria, hatujasajiliwa chini ya Wizara inayohusika na mambo ya ajira,” ameongeza.
Akikumbushia juu ya Waraka wa Baba Mtakatifu Leo XIII uitwao ‘Rerum Novarum’, Askofu Dallu ameeleza kuwa kuna haja ya kujikita katika mfumo wa elimu unaolenga kujenga dhamiri za wasomi, ili kuliepusha Taifa dhidi ya watumishi wasio waadilifu.
Marufuku kubinafsisha karama
Pia Askofu Dallu ametoa angalizo kwa Vyama vya Kitume na waamini nchini kutobinafsisha karama, na badala yake kumtambulisha Kristo kupitia yale yote wanayoyafanya. Ameonya tabia ya watu kutaka kuonekana wao katika mambo wanayoyafanya na kumuweka pembeni Kristo, jambo linalochochea dharau dhidi ya viongozi wa kiroho.
“Kupitia karama zenu hakikisheni mtu anamuona Kristo na siyo ninyi. Chochote mnachokifanya ni lazima aonekane Kristo kwanza. Msitumie karama kufanya biashara. Na isitokee watu wanasali kwa ajili ya kuponywa tu, matokeo yake tutakuwa na makanisa ya wagonjwa, kwani wote watakaohudhuria watakuwa wagonjwa isipokuwa yule anayeombea. Huu ni mwanzo wa wakristo kuwa watumwa wa mwombeaji, na ni kinyume na maagizo ya Kristo ambaye alipowaponya watu aliwaambia waende zao,” ameeleza.
No comments: