SIKU YA MT.INYASI WA LOYOLA

Mama Kanisa ameadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, hapo tarehe 31 Julai 2017 kwa kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na utukufu; kwa upendo wake wenye huruma, kwa watu wote. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanayataka Mashirika yote ya kitawa kuwa aminifu kwa karama za mashirika yao ambayo kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa. Waanzilishi wa Mashirika haya, walionja na kuguswa na huruma ya Mungu katika maisha yao. Kumbe, kila karama ya Shirika ni zawadi ambayo Roho Mtakatifu anaitoa kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Katika mazingira kama haya, karama ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola inapaswa kupyaisha na kuendelezwa kwa kusoma alama za nyakati, ili kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashuhudia upendo huu kwa kufuata Amri za Mungu; sanjari na kumpenda Mungu na jirani. Kwa Wayesuit, wanapaswa kujenga na kudumisha urafiki wa dhati na Kristo Yesu, ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wake; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa Kristo na Kanisa lake! Urafiki na upendo huu, unapaswa kujikita katika sakafu ya maisha ya mwamini, kama kifungo cha upendo wa dhati.
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika la Wayesuit wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Wayesuit kama walivyo waamini wengine ndani ya Kanisa, wanahamasishwa kukita maisha yao katika tafiti, elimu na ufahamu makini wa binadamu ili kusaidia kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Shirika la Wayesuit anasema Padre Sosa, linajitahidi kuwekeza zaidi katika majiundo awali na endelevu katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, ili kuwawezesha Wayesuit kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa mataifa, tamaduni na nyakati zote.
Kipaumbele cha kwanza ni sifa na utukufu anaopaswa kupewa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Moyo ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anapenda kukutana na kuzungumza na waje wake, kumbe kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, Hekalu la Mungu linakuwa ni safi, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu, ili waweze kuwaongoza waja wake. Waamini wanakumbushwa kwamba, yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, aliyewapatanisha na Nafsi yake kwa njia ya Kristo Yesu na hatimaye, kuwakirimia huduma ya upatanisho. Huu ni mwaliko wa kuendelea na hija kuelekea katika chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu.
Itakumbukwa kwamba, Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika la Wayesuit alichaguliwa tarehe 14 Oktoba 2016 na wajumbe kutoka katika Kanda 85 na tayari amekwisha kutembelea: India, Perù, Hispania, Ujerumani, Rwanda, Burundi, DRC., Kenya, Indonesia, Cambordia na sasa anapanga pia kutembelea Ubelgiji, ili kukutana na kusalimiana na ndugu zake katika Kristo Yesu. Anasema, kwa wakati huu wasi wasi umetenda nchini Venezuela kutokana na machafuko ya kisiasa kama walivyoshuhudia wakuu wa Kanisa. Kura ya Maoni iliyoitishwa na Serikali ya Raia Nicholàs Maduro, imewashirikisha watu zaidi ya milioni saba, tukio la aina yake katika historia ya Venezuela, jambo la msingi kwa wakati huu ni kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano ya kitaifa; siasa iwe ni kwa ajili ya huduma ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si fujo na ghasia.
Anasema, maisha na utume wake kama Mkuu wa Shirika yana changamoto zake, kwani kuna mambo ambayo hayana budi kutolewa maamuzi kwa wakati muafaka, kwa njia ya ushirikiano na washauri wa kuu wa Shirika. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Shirika linaendeleza karama yake kwa kusoma alama za nyakati, daima likijitahidi kuipyaisha, kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano; kwa kujikatalia, ili kuwa na kiasi; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuendelea kuwa tayari kuitikia na kutekeleza mahitaji ya Kanisa la Kristo kama yanayofafanuliwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ikumbukwe kwamba, Wayesuit wanaweka nadhiri ya utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Padre Arturo Sosa, Mkuu wa Shirika la Wayesuit anakaza kusema, maisha na utume wao kwa nyakati hizi ni: Upatanisho na Mwenyezi Mungu, Binadamu na Mazingira. Wanatambua kwamba, wao ni washiriki na wadau wakuu wa maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani na kwamba wao pia ni sehemu ya Kanisa, wanaotumwa duniani kusimama kidete: kulinda, kutetea: utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi kwa kujikita katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Upatanisho unafumbatwa katika mchakato wa majadiliano: katika ukweli na uwazi. Haya ni majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi. Utume wa upatanisho unasimikwa katika maisha ya mtu binafsi, jumuiya na Kanisa katika ujumla wake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

2 comments:

Powered by Blogger.