Serikali yasisitiza Bunge kutooneshwa mubashara.

Na Damasus Mtalaze, Kibakwe

SERIKALI imeendelea kusisitiza kuwa azma yake ya kutokuonesha Bunge moja kwa moja kuwa ni kutokana na matumizi ya lugha zisizofaa za matusi na badala yake itaendelea kuonesha vipindi vya Bunge sehemu ya maswali na majibu kwani eneo hilo linawafaa watanzania wote kwa sababu wanapata majibu ya moja kwa moja ya Serikali kwa matatizo yanayowakabili .
Hayo yamesemwa na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI Mhe George Simbachawene katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Pwaga wilayani Mpwapwa hivi karibuni.
Waziri Simbachawene amesema kuwa baada ya Serikali kuona lugha zisizofaa zikitolewa bungeni, imeona si vyema kuonesha Bunge moja kwa moja kwa sababu lugha nyingi zisizofaa haziwafai watanzania kwani hazifundishi zaidi ya kupotosha na kuharibu maadili mema yaliyojengeka katika jamii na hasa kwa watoto.
Mhe. Simbachawene amesema kuwa Serikali imeona ni vyema kuzuia Bunge zima kuoneshwa na badala yake kuoneshwa vipande vya maswali na majibu kwa sababu hakuna lugha zisizofaa zinazotolewa sehemu hiyo na kuwa sehemu hiyo Serikali inapata nafasi ya kuwajulisha watanzania kuhusu utatuzi wa shida zao kutokana na swali la Mbunge mhusika aliyetaka kujulishwa tatizo la wananchi wake .
“Watanzania wenzangu mtu anasimama anamtukana Mbunge mwenzake, mnataka Serikali ioneshe, Mbunge anamtukana waziri Serikali ioneshe, Mbunge anamtukana Rais, sisi wabunge tutakuwa tunawafundisha nini watoto wetu? watoto wakikosa maadili mema nani wa kulaumiwa kama siyo sisi wabunge tunaotunga sheria?” amehoji Waziri Simbachawene.
Amesema watanzania wana shida zinazohitaji utatuzi na si lugha chafu au matusi. Ameongeza kuwa siku zote maneno yasiyofaa hayaifai nchi na badala yake yanabomoa na kuwatoa watanzania kwenye umoja, mshikamano, upendo na udugu wao . Amesema utawala wa awamu ya tano hautakubali tunu hizo zipotee kwa kufumba macho kama vile Serikali haioni madhara yake, kwani lugha za matusi si maadili ya watanzania.
Kuhusu tatizo la maji kwa kijiji cha Pwaga, amemwagiza Mkurugenzi wa wilaya hiyo Bwana Mohamed Maje kuwa wale wote walio katika vyanzo vya maji wawe wamehamishwa ndani ya siku 14 na kuwa taarifa hiyo iwasilishwe ofisini kwake haraka. Amesema ni vyema kupata ufumbuzi huo mapema ili watu wasiendelee kuteseka wakati waharibifu wapo wanaonekana.
“Maeneo ya vyanzo vya maji yasipotunzwa watanzania watateseka, kwa hiyo ni vyema kujihadhari mapema kabla maisha ya watanzania hayajafikia pabaya.” amesisitiza Mheshimiwa Simbachawene .

No comments:

Powered by Blogger.