NA ASKOGU DALLU ASEMA ANAUNGANA NA RAIS WATOTO WANAOPATA MIMBA KUTOENDELEA NA MASOMO
Ask Dallu
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea Mhashamu Damian Dallu amesema kuwa anaunga mkono hatua ya Rais John Magufuli kutoruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo, na kusema kuwa shule zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki hazitaruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo.
Amesema hayo katika Ibada ya Misa Takatifu ya Upadrisho wa Shemasi Jerome Mtatifikolo, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria Afya ya wagonjwa Ilole jimboni Iringa ambapo amebainisha kuwa wanaoshabikia wanaopata mimba kurudi shule wanaharibu utamaduni wa kiafrika na kuchafua heshima ya Taifa.
“Hayo mambo siyo sehemu ya utamaduni wetu wa Afrika, ni mambo ya kigeni yanayotaka kutuchafulia utamaduni wetu. Nawashangaa eti wanapigania haki ya tendo la ndoa, haki ya wapi hiyo?. Tutakuwa na shule za namna gani zinazoruhusu mwanafunzi kwenda kulea mtoto kisha arudi tena na akipata mimba nyingine aende tena nyumbani?” Amehoji Askofu Dallu.
Katika hatua nyingine Askofu Dallu amewaasa waamini kufanya maandalizi ya kutosha hasa ya kiroho wanapojiandaa kuingia katika Sakramenti ya Ndoa ili ndoa zao ziwe na mwelekeo wa kiimani zaidi. Amesema kuwa kabla ya kupewa upadri, Shemasi Jerome alihudhuria mafungo ya kiroho ya siku 5 jambo ambalo linapaswa kuigwa na wale wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya ndoa badala ya kujikita katika kufanya maandalizi ya kimwili.
“Watu wa familia mnatumia siku ngapi kufanya mafungo kabla ya kufunga ndoa? Au ndiyo ile kufanya maandalizi mengine ya kimwili marefu. Mkumbuke kuwa hata sisi mapadri tunatoka kwenu, matokeo ya kukosa maandalizi ya kutosha kabla ya ndoa ndiyo haya tunayoshuhudia sasa hivi ambapo wanaoishi ndoa kama Sakramenti ni wachache,” ameeleza.
Aidha amesema kuwa watu wanaoishi maisha ya pamoja kwa muda mrefu hadi kuwa na watoto hawastahili kuitwa wachumba kwa kuwa uchumba kielelezo chake ni Maria na Yosefu, na kuwataka kuacha kutumia jina hilo na badala yake wajiite wachumba sugu.
“Ulisikia wapi watu wanaishi uchumba mpaka wanakuwa na wajukuu? Tafuteni jina jingine kuanzia sasa labda mjiite wachumba sugu. Tutapata mapadri na masista wa namna gani? Kielelezo cha uchumba ni Yesu na Maria,” Ameeleza.
Pia amesema kuwa kazi ya karama ni kujenga umoja wa Kanisa na siyo kuligawa, na kumtaka kila mmoja kutumia wito wake kumtajirisha mwingine.
No comments: