MASOMO YA MISA, JANUARI 9, 2018
JUMANNE, JUMA LA 1 LA MWAKA

SOMO 1
1Sam. 1:9-20

Walipokwisha kula na kunywa huko Shilo Hana akainuka. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwino wa hekalu la Bwana. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana, akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.
Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. Hana akajibu, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni; mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena.
Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana.

Neno la Bwana…

WIMBO WA KATIKATI
1Sam. 2:1,4-5,6-7,8 (K)1

(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana.

Moyo wangu wamshangilia Bwana,
Pembe yangu imetukuka katika Bwana,
Kinywa change kimepanuka juu ya adui zangu,
Kwa kuwa naufurahia wokovu wako. (K)

Pinde zao mashujaa zimevunjika,
Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba,
Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. (K)

Bwana huua, naye hufanya kuwa hai;
Hushusha hata kuzimu tena huleta juu.
Bwana hufukarisha mtu naye hutajirisha;
Hushusha chini tena huinua juu. (K)

Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Humpandisha mhitaji kutoka jaani,
Ili awaketishe pamoja na wakuu,
Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu,
Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana. (K)

SHANGILIO
1Tim. 2:13

Aleluya, aleluya,
Lipokeeni Neno la Mungu, siyo kama neno la wanadamu, bali kama Neno la Mungu.
Aleluya.

INJILI
Mk. 1:21-28

Yesu na wanafunzi wake walishika njia mpka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akifundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.
Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.

No comments:

Powered by Blogger.