MASOMO YA MISA 11 JANUARI 2018 ALHAMISI JUMA LA KWANZA LA MWAKA

SOMO 1:1Sam.4:1-11

Ikawa siku zile Wafilisti walikusanyika ili kupigana na Israeli, nao Waisraeli wakatoka juu ya Wafilisti kwenda vitani; wakatua karibu na Ebenezeri, nao Wafilisti wakatua huko Afeki. Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani wapata watu elfu nne.
Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona, Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la agano la Bwana toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu. Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la agano la Bwana wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la Mungu. Na sanduku la agano la Bwana lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma.
Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la Bwana limefika kambini. Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo. Ole wetu; ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamistri kwa amapigo ya kila namna jangwani. Iweni hodari, na kufanya kiume, enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao.
Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 44:9-10,13-14,23-24 (K) 26

(K) Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.

Lakini umetutupa umetufedhehesha,
Wala hutoki na majeshi yetu.
Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo,
Na watuchukiao wanajipatia mateka. (K)

Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu,
mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa,
Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi. (K)

Amka, Bwana, mbona umelala?
Ondoka, usitutupe kabisa,
Mbona unatuficha uso kwako,
Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu. (K)

SHANGILIO
Mt. 4:23

Aleluya, aleluya,
Yesu aliihubiri Habari njema ya ufalme, na kuponya udhaifu wa kila namna katika watu.
Aleluya.

INJILI:Mk.1:40-45


Siku ile mtu mwenye ukoma akaja kwa Yesu, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.
Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.

Neno la Bwana… Sifa kwako ee Kristu.

No comments:

Powered by Blogger.