MASOMO YA MISA 18 JANUARI 2018 ALHAMISI JUMA LA PILI LA MWAKA

SOMO 1:1Sam.18:6-9;19:1-7

Walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.
Nao wale wanawake wakitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akagadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elf utu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.
Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi. Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na DAudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, uiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha; na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lolote nitakuambia.
Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye, akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi; kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure?
Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa. Basi Yonathani akamwita Daudi aje, Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta kwa Sauli, naye alikuwa akihudhuria mbele yake, kama kwanza.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 56:1-2, 8-12 (K)

(K) Nimemtumaini Mungu sitaogopa.

Mungu, unirehemu, maana yuko atakaye kunimeza,
Mchana kutwa ananionea akileta vita.
Adui zangu wanataka kunimeza mchana kutwa,
Maana waletao vita yangu kwa kiburi ni wengi,
Ee Mungu wangu. (K)

Umehesabu kutangatanga kwangu,
Uyatie machozi yangu katika chupa yako,
Je! Hayamo katika kitabu chako?
Ndipo adui zangu watarudi nyuma,
Siku hiyo niitapo. (K)

Neno hili najua kuwa Mungu yu upande wangu.
Kwa msaada wa Mungu nitalisifu neno lake,
Kwa msaada wa Bwana nitalisifu neno lake. (K)

Nimemtumaini Mungu,
Sitaogopa mwanadamu atanitenda nini?
Ee Mungu, nadhiri zako zi juu yangu,
Nitakutolea dhabihu za kushukuru (K)

SHANGILIO
Zab. 119:135

Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya. 

INJILI:Mk.3:7-12

Yesu alijitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa. Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. Akawakataza sana, wasimdhihirishe.


Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

No comments:

Powered by Blogger.