MASOMO YA MISA JUMA LA 31 LA MWAKA WA KANISA JUMANNE,7 NOVEMBA 2017

SOMO 1:Rum.12:5-16

Sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya Imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia, kwa bidi; mwenye kurehemu, kwa furaha.
Pendo na lisiwe na unafiki; lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu; kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni, mkijitahidi.
Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani. Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao. Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 131

(K) Moyo wangu uwe na Amani kwako, Ee Bwana.

Bwana, moyo wangu hauna kiburi,
Wala macho yangu hayainuki.
Wala sijishughulishi na mambo makuu,
Wala na mambo yashindayo nguvu zangu. (K)

Hakika nimeituliza nafsi yangu,
Na kuinyamazisha.
Kama mtoto aliyeachishwa
Kifuani mwa mama yake;
Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu. (K)

Ee Israeli, umtarajie Bwana,
Tangu leo n ahata milele. (K)


SHANGILIO
Zab. 147:12,15

Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.


INJILI:Lk.14:15-24


Mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja na Yesu alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu. Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.
Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya miji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, n ahata sasa ingaliko nafasi.
Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.

No comments:

Powered by Blogger.