MASOMO YA LEO IJUMAA JUMA LA 26 LA MWAKA WA KANISA 6 OCTOBA 2017

SOMO 1:Bar.1:15-22

Kwa Bwana Mungu wetu, haki; lakini kwetu sisi haya ya uso kama hivi leo, kwa watu wa Yuda na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kw awafalme wetu, na kwa wakuu wetu, na kwa makuhani wetu, na kwa manabii wetu, na kwa baba zetu, kwa sababu tumetenda dhambi mbele ya Bwana. Tumemwasi, wala hatukuitii sauti ya Bwana Mungu wetu, kwenda katika sheria zake alizoziweka mbele yetu. Tangu siku Bwana aliyowatoa baba zetu katika nchi ya Misri hata leo tumemwasi Bwana Mungu wetu na kutenda yasiyofaa kwa kutoisikiliza sauti yake.
Kwa hiyo mapigo haya yameshikamana nasi, na ile laana ambayo Bwana alimwamuru mtumishi wake Musa, katika siku aliyowaleta baba zetu kutoka katika nchi ya Misri ili atupe nchi ijaayo maziwa na asali, kama hivi leo. Lakini hatukuisikiliza sauti ya Bwana Mungu wetu, kwa kuyafuata maneno yote ya manabii aliyotupelekea, bali tulikwenda kila mtu katika mawazo ya moyo wake mbaya, kutumikia miungu ya kigeni na kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana Mungu wetu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 79:1-6, 8-9 (K) 9

(K) Utusaidie, Ee Mungu, kwa ajili ya utukufu wa jina lako.

Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako,
Wamelinajisi hekalu lako takatifu.
Wamefanya Yerusalemu chungu chungu.
Wameziacha maiti za watumishi wako
Ziwe chakula cha ndege wa angani.
Na miili ya watauwa wako Iwe chakula cha wanyama wa nchi. (K)

Wamemwaga damu yao kama maji
Pande zote za Yerusalemu,
Wala hapakuwa na mzishi.
Tumekuwa lawama kwa jirani zetu,
Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira milele?
Wivu wako utawaka kama moto? (K)

Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima.
Kwa maana tumedhilika sana. (K)

Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K)

SHANGILIO
Yn. 10:27

Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.

INJILI:Lk.10:13-16

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.


No comments:

Powered by Blogger.