MASOMO YA JUMA LA 28 LA MWAKA IJUMAA 20 OKTOBA 2017

SOMO 1:Rum.4:1-8


Tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili? Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu. Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki. Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni. Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, Imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki. Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,
Heri waliosamehewa makossa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 32:1-2.5.11 (K) 7

(K) Ni wewe sitara yangu, Ee Bwana.

Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makossa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
Ambaye rohoni mwake hamna hila. (K)

Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. (K)

Mfurahieni Bwana;
Shangilieni, enyi wenye haki.
Pigeni vigelegele vya furaha;
Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo. (K)


SHANGILIO
Zab. 130:5

Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.


INJILI:Lk.12:1-7


Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki. Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana. Basi, yoyote mliyosema gizani yatasikiwa mwangani; na mliyonena sikioni mwa mtu katika vyumba vya ndani, yatahubiriwa juu ya dari.
Name nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda Zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa, mwogopeni yule ambaye akiishakumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanam; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo. Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.



   

No comments:

Powered by Blogger.