AINA ZA SADAKA!.
Zipo Aina kadhaa za Sadaka, lakini mimi nitaelezea Aina sita za Sadaka!. Aina hizo ni:

1)MALIMBUKO
Malimbuko huitwa "first fruits", yaani mazao ya kwanza!.
Chochote kile cha Kwanza, katika vile unavyozalisha ni Malimbuko Mbele za Bwana, mfano, Mshahara wako wa kwanza, Mazao yako ya kwanza, Faida ya kwanza katika biashara yako!.
Wana wa Israeli waliambiwa watoe Mazao yao ya kwanza pale watakapokanyaga nchi, watakayopewa na Bwana Mungu!.
(Kumbu 26:2),
Kutoa Malimbuko, ni kumuheshimu Mungu (Mithali 3:9-10).
Malimbuko, humruhusu Mungu kuweka ulinzi katika eneo husika ulilotoa limbuko hilo, kama biashara, mazao, mifugo n.k!.

2)DHABIHU.
Dhabihu ni sadaka ya hiari, ambayo Mtu anamtolea Mungu, Makanisani huitwa Sadaka ya Kawaida, ambayo Mtu hupangiwi kiwango cha kutoa,
Kwa kurahisisha huitwa tu sadaka,
Mtoaji anaweza akaitoa kwa ajili ya Ndoa yake, familia yake, Masomo yake, n.k.
(Zaburi 50:4,14).
Mtu anaweza kuutoa Mwili wake kama Dhabihu, Mungu ameagiza kuitoa Miili yetu iwe dhabihu!.

3)ZAKA
Zaka ni Sehemu ya kumi ya mapato yako, wengine huita Fungu la Kumi, 10%.
Mtu unapopata Mshahara, au faida kwenye Biashara yako Sehemu ya Kumi ni ya Mungu,
Mfano, ukipata Tsh.
10,000/=, ujue Tsh 1,000/= ni ya Mungu, lazima uipeleke Madhabahuni kwa Bwana!.
(MALAKI 3:10),
Kama ukipunguza sehemu ya Kumi ya Mapato yako, au usipotoa Kabisa, unaitwa Mwizi (MALAKI 3:8),
Kama Ukizidisha kutoa, mfano umepata Tsh. 1,000/=, fungu la kumi ni Tsh 100/=, wewe badala ya kutoa Tsh. 100/=, Ukatoa Tsh. 200/=, Ujue, Zaka ni 100/=, ndio sehemu takatifu ya Mungu, hiyo uliyozidisha, inakua Dhabihu (Hata kama zote, umeziweka kwenye Bahasha Moja).
Tayari nimeshazielezea Aina tatu hivi za Sadaka, na sasa hivi namalizia aina Zingine tatu,

4)NADHIRI.
Nadhiri maana yake ahadi, Ni sadaka ambayo Mtu anaitoa kwa Maneno!.
Mfano, unaweza kumwambia Mungu, Mungu ukinipa Kazi, Mshahara wangu wa miezi Mitatu ya Kwanza nitakupa!.
Ujue hiyo ni nadhiri, kwa hiyo Mungu akikipa Kazi, Ujue Mshahara wa Miezi mitatu ya kwanza, sio wako, ni wa Mungu!.
Tena, Ukimwambia Mungu, Mungu Nikipata Mme/Mke mwaka huu, ntakupa Ng'ombe,
Ndani ya Mwaka huu, ukipata, Ujue unatakiwa Kutoa Ng'ombe!. Lakini kama hujapata ndani ya Mwaka huu, Basi upo huru kutoa,au kutotoa!.
Nadhiri ni Mkataba wako na Mungu, Mungu Akifanya Unalipa, asipofanya Upo huru, waweza kulipa au Usilipe!.
MAMBO YA MUHIMU KUJUA, KUHUSU NADHIRI
👉Ukiweka nadhiri, Usikawie kuiondoa!.
MHUBIRI 5:4
"Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri."
👉Usipoiondoa, inakua Dhambi!.
KUMB 23:21-23
"Utakapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakua dhambi kwako. Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakua dhambi kwako. Yaliyotoka mdomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri BWANA, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako."
Unapofanya Maombi, wakati wa shida, ni rahisi sana kumuwekea Mungu nadhiri, na Mungu ni mwepesi sana kukujibu, ili aipate sadaka yako, lakini kukumbuka Nadhiri uliyoiweka ndio kazi iliyopo, Ndio maana ni afadhali, usiweke nadhiri, kuliko kuiweka, na Usiitimize!!!.

5)SHUKURANI
Sadaka hii, ni sadaka ya kawaida kabisa, ambayo niliita dhabihu, lakini hii hutolea kwa lengo la kumshukuru Mungu, kwa jambo alilokufanyia!.
Hutolewa, ili kumtukuza Mungu, baada ya kuvuka hatua flani!.
ZABURI 50:23a
"Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza."
Unaweza ukaitoa, baada ya Kumaliza elimu ya Msingi, au Elimu ya Sekondari, au unaweza ukaitoa baada ya Kufauli mitihani, au kuoa/kuolewa n.k
MGAWANYIKO WA SADAKA YA SHUKURANI.
I) Isiyo na Nadhiri
II)Yenye nadhiri
I)ISIYO NA NADHIRI
hutolewa bila ahadi, hutolewa tu baada ya Mungu kufanya Jambo katika Maisha yako!.
Mfano, Ukisoma Kutoka 18:8-12, Utakutana na habari za Musa, na Yethro Mkwewe.
Baada ya Mungu kuwavusha watu wake, Yethro akatoa sadaka ya Shukranu.
II)YENYE NADHIRI
Hii, hutolewa kwa ahadi. Mfano, ukisema Mungu nikipata Mtoto, nitakutolea Sadaka ya Shukurani, Mungu akikupa Mtoto, ukienda kutoa Sadaka ya Shukurani, ujue hiyo ni Sadaka ya Shukurani, yenye Nadhiri (unatimiza nadhiri yako).

6)MBEGU
Nafikiri unaijua Mbegu, Mtu anapanda Mbegu, ili apate Mazao, sasa ipo sadaka, inaitwa Sadaka ya Mbegu.
Sadaka hii, unaipanda Madhabahuni, au sehemu flani/ kwa mtumishi, ukiwa na tarajio flani, kupitia hiyo sadaka!.
Mara nyingi watu hutoa sadaka hii kwa ajili ya Biashara, Kazi, Afya, Familia n.k.
Sio, lazima Mtu akwambie Njoo upande Mbegu Madhabahuni kwa Bwana, ni wewe mwenyewe unasikia Moyoni mwako Kupanda Mbegu Madhabahuni/ kwa huyo Mtu.
Mtu akikupangia kiwango cha Mbegu, au aina ya Mbegu kwa lengo la kujinufaisha, huyo ni TAPELI MKUBWA, hata Kama anaitwa MTUME NA NABII!.
Zingatia hili;
"Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu". 2KOR 9:6,7
Pia, Soma Wagalatia 6:7.
HIZO NI BAADHI YA AINA ZA SADAKA, MUNGU ALIZONIJAALIA KUZIFUNDISHA KWENYE SOMO HILI!.
KUMBUKA: Tunatoa Sadaka kwa Imani, Msingi wake ukiwa ni Upendo wa Mungu ndani yako,
Maana Ukitoa Bila kuwa na Upendo, ni Bure (1 Korintho 13:3)

No comments:

Powered by Blogger.