MASOMO DOMINIKA YA 27 YA MWAKA 8 OKTOBA 2017

MWANZO:

Est. 13:9, 10-11
Ee Bwana ulimwengu wote u katika uweza wako, wala hakuna awezaye kukupinga ukipenda. Wewe umeumba yote, mbingu na nchi na vitu vyote vya ajabu vilivyomo chini ya mbingu; ndiwe Bwana wa yote.


SOMO 1:Isa.5:1-7

Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu.
Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi walio wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; nami nitaliharibu, wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinye mvua juu yake. Kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 80:8, 11-15, 18-19, (K) Isa. 5:7

(K) Shamba la mizabibu la Bwana, ndilo nyumba ya Israeli.

Ulileta mzabibu kutoka Misri,
Ukawafukuza mataifa ukaupanda.
Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini,
Na vichipukizi vyake hata kunako mto. (K)

Kwa nini umezibomoa kuta zake,
Wakuchuma wote wapitao njiani?
Nguruwe wa msituni wanauharibu,
Na hayawani wa kondeni wanautafuna. (K)

Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu,
Na mche ule ulioupanda,
Kwa mkono wako wa kuume. (K)

Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.
Ee Bwana, Mungu wa majeshi, uturudishe,
Uangazishe uso wako nasi tutaokoka. (K)

SOMO 2:Flp.4:6-9

Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.


SHANGILIO
Yn. 10:27

Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, asema Bwana; Nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.


INJILI:Mt.21:33-43

Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampigam na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile. Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu?
Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa linguine lenye kuzaa matunda yake.

No comments:

Powered by Blogger.