UKIMYA WA KaNISA KATOLIKI UTAWAPOTEZA WAUMINI
Lijibu changamoto za sasa kupitia sayansi na teknolojia
Na Thompson Mpanji,Mbeya
MKURUGENZI wa Radio Vatikani, Sean Patrick Lovett amelialika Kanisa Katoliki Tanzania kujenga utamaduni wa mawasiliano kwa kutumia vyombo vya habari mahalia kuendana na Sayansi na Teknolojia ili kufikisha mafundisho na ujumbe wa Viongozi wakuu wa Kanisa kwa waamini.
Mkurugenzi huyo amesema hayo wakati wa semina iliyowahusisha mapadri,Watawa wa kike na kiume, mafrateri, viongozi wa Parokia,Wakurugenzi na baadhi ya wafanyakazi wa Idara za Jimbo Katoliki la Mbeya iliyofanyika Septemba mosi 2017 katika Ukumbi wa Parokia ya Mbeya Mjini.
Sean amesema kuwa ni jukumu la Maaskofu, Maparoko,Wakuu wa Mashirika,Wakurugenzi wa Idara mbalimbali, Viongozi wa Parokia na Halmashauri za Walei sanjari na vyama vya kitume kuvitumia vyombo vya habari vya Kanisa na waandishi wake kufikisha ujumbe na mafundisho ya Kanisa.
Huku akitolea mfano wa Baba Mtakatifu Francisko alivyokuwa wazi kuendana na ulimwengu wa kidijitali kwa kutumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe ikiwemo kuzungumza na kila mtu duniani kwa muda mfupi kupitia Twitter, Instagram, Face book na vyombo vingine vya habari vivyo hivyo kwa Viongozi wa Kanisa mahalia na waamini wanapaswa kuiga mfano huo.
“Tunajaribu kumuona Papa Francisko alivyofungua mitandao ya kijamii ili kuendana na sayansi na Teknolojia …kuendana na wakati na mahitaji ya sasa, amekuwa akitumia na kujiwekea muda wa kuwasiliana na kila mtu kupitia mitandao na vyombo vya habari na hivi ndivyo Kanisa la Tanzania na la kiulimwengu linapaswa kufanya”.
“Tuangalie wengine hususani waamini wetu na kuwapa mahitaji yao ya kiroho kwa haraka na ukarabu kupitia vyombo vya habari vya Kanisa.
Lazima tuwe wazi tusijifungie kwani ulimwengu umebadilika, kwa hiyo tukiwa hatuwi wazi kuwapatia mafundisho kupitia mitandao na vyombo vya habari,kufikisha ujumbe wa Kanisa na maandiko zikiwemo Sheria na Taratibu za Kanisa ….watakwenda kuangalia na kusikia kwa wengine na matokeo yake tutawapoteza, hivyo mawasiliano na kutumia vyombo vyetu na waandishi wetu ni muhimu kwa sasa kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo katika Kanisa,”amesisitiza Mkurugenzi huyo.
Aidha amezungumzia umuhimu wa majimbo kuanzisha vyombo vya habari ikiwemo Radio, Televisheni, Magazeti na mitandao ya kijamii ikiwemo Tovuti za majimbo na blogs ili waamini waweze kuendelea kupata habari, mafundisho na ujumbe wa Kanisa.
Hata hivyo washiriki wa semina hiyo wamepongeza msimamo na muelekeo huo wa Kanisa Katoliki kwa mahitaji ya sasa badala ya kuwepo kwa ukimya ambao watoto na vijana wanaweza kushindwa kulielewa vyema Kanisa lao na hatimaye kuweza kukengeuka na kukimbilia katika madhehebu.
Katika semina hiyo Askofu Evarist Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya alionesha kufurahishwa na mafundisho hayo huku Mkurugenzi huyo akimshukuru Askofu kwa kumwalika kutoa semina hiyo ambayo ni muhimu kwa Kanisa Katoliki duniani kuendana na mahitaji ya sasa kwa afya ya Kanisa kwa ujumla.
No comments: