NOVENA YA ROHO MTAKATIFU

NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA KWANZA, IJUMA

ROHO MTAKATIFU ANATUFARIJI



Yesu alipokuwa akiagana na mitume wake, kabla ya kupaa mbinguni, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu mpaka hapo watakapokuwa wamempokea Roho Mtakatifu. Aliwaambia: “Wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni, mtajazwa nguvu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika nchi yote ya Yuda na Samaria, hata kwenye mipaka yote ya dunia.” (Mdo.1:8)

Waliendelea kusali pamoja toka hapo Yesu alipopaa mbinguni mpaka siku ya Pentekoste. Waliomba Roho Mtakatifu awashukie, awajaze na mapaji yake. Na baada ya siku tisa Roho Mtakatifu aliwashukia hao kundi dogo nao wakawa chanzo cha Kanisa lililopata kuenea duniani kote.

Siku hizo tisa za kusali zinaitwa NOVENA; na kila mwaka wakati huu, wakristu wakifuata mfano wa mitume, wanasali muda wa siku tisa kabla ya Sikukuu ya Pentekoste. Wanamuomba Roho Mtakatifu awashukie, awajaze nguvu na wingi wa mapaji yake.

Wakati huu wa NOVENA ,  Tunayo mengi ya kuliombea Kanisa na kujiombea sisi wenyewe. Kwa hiyo tumuombe Roho Mtakatifu atusaidie kusali vema na kuomba yale yote tunayohitaji kwa maslahi yetu ya roho na mwili.

Na kama mtume Paulo alivyowaambia wale waKristu wa kwanza, Roho Mtakatifu huja kutufatiji katika udhaifu wetu. Basi tumuombe atufariji kwa sala hizi za NOVENA, Atuwezeshe kusali na kuomba inavyotupasa kusali.

1.       Ee Baba wa milele, tunakuomba umtume Roho Mtakatifu atushukie sisi taifa lako awashe ndani yetu moto wa upendo wako.
W. Twakuomba utusikie.

2.       Ee Baba mwema, tunakuomba utujalie faraja ya Roho Mtakatifu sisi wana tulio katika dhiki na taabu nyingi mno hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.

3.       Ulijalie Kanisa lako mapaji ya Roho wako Mtakatifu, liweze kutekeleza vema utume wake wa kuhudumia watu wote hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.

4.       Utujalie sisi kudumu katika NOVENA hii mpaka mwisho kama Maria na mitume walivyodumu pamoja wakisali kabla ya Pentekoste ile ya kwanza.
W. Twakuomba utusikie.

5.       Utujalie neema zote zinazohitajika ili tuweze kumshuhudia Kristu popote kwa mwenendo na matendo yetu ya kila siku, tukiongozwa na Roho Mtakatifu.
W. Twakuomba utusikie

6.       Uzijalie familia zote za wakristu neema na nguvu za Roho Mtakatifu tupate kuendelea pasipo kuchoka katika sala na katika matendo mema siku zote.
W. Twakuomba utusikie

7.       Ewe Roho Mtakatifu, uwajalie vijana wetu moyo wa ujasiri, wapate kulijenga kanisa lako na kueneza utawala wako katika jumuia zetu za Kikristu.
W. Twakuomba utusikie.

TUOMBE;
Ee Mungu, uliye muumba wa vitu vyote ,  tunakuomba utusikilize kwa wema sala zetu sisi taifa lako, utuongoze sote tufuate siku zote utaratibu wa mapenzi yako; naye Roho Mtakatifu atutegemeze mpaka mwisho wa novena hii. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu .
W. Amina.

No comments:

Powered by Blogger.