WAWATA HIMIZENI MIITO
“WAWATA HIMIZENI MIITO”
WITO umetolewa kwa wanawake wakatoliki nchini kuhimiza miito mitakatifu kuanzia ngazi za familia, jumuiya ndogo ndogo,vigango, parokia hadi majimboni ili Kanisa liweze kupata hazina kubwa ya mapadri na masista watakaolitumikia kimwili na kiroho pamoja na watu wake.
Aidha imeelezwa kuwa mapadri na masista waliopo umri unazidi kuongezeka na hivyo Kanisa linahitaji vijana wa kike na kiume watakaoandaliwa katika malezi na kusomeshwa katika Seminari mbalimbali ili waweze kushika majukumu ya kichungaji na kitume katika Kanisa mahalia.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Wanawake Wakatoliki Taifa(WAWATA) ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA Jimbo Kuu Dar es Salaam, Bi.Desderia Mahita wakati wa hitimisho la Kongamano la siku tatu la Kanda ya Nyanda za Juu Kusini lililofanyika jimboni Mbeya na kuwashirikisha wanawake wa majimbo 8 ya Jimbo Kuu Katoliki Songea.
Majimbo ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika Jimbo Kuu Songea yaliyoshiriki katika Kongamano hilo tangu Juni 23 hadi 25 ni pamoja na Jimbo Katoliki Mbeya, Lindi, Mtwara, Tunduru Masasi, Njombe, Iringa, Mbinga na Songea lenyewe ambapo zaidi ya wanawake 1000 walishiriki.
Katibu huyo ambaye ni mlezi wa WAWATA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini amewaalika wanawake wote kuwa wanapohitimisha Kongamano hilo wabebe jukumu la kwenda kuhimiza miito mitakatifu katika familia zao na jumuiya ndogo ndogo.
“Akina Mama ni jukumu letu kwenda kuhimiza miito mitakatifu, chukueni hiyo kazi na mjiulize je Jumuiya, Kigango, Parokia na Jimbo lina mapadri na masista wangapi na mkawahimize watoto waende seminari isiwe kwa fasheni bali mkaguswe mioyoni mwetu na tuombe baraka za Mwenyezi Mungu tuishi maisha ya familia takatifu kama ya Yesu, Maria na Yosefu, tuhimizane na tukahimizane kufunga na kubariki ndoa,”amesisitiza.
“Wanawake Wakatoliki tuwe wakamilifu yaani tusiwe eti misa ya kwanza tunasali kanisani na misa ya pili tunaenda kwenye maombi katika madhehebu ambako tunakatazwa kuvaa rozari na tunakatiwa na rozari…lakini tuwe watu wa msamaha, sisi wanandoa enzi zetu wakati tunafanyiwa mafundisho ya ndoa tulikuwa tunafundishwa na mababa kuwa tukigombana ndani ya nyumba tuhakikishe tunapatana kabla ya jua halijazama,” amefafanua Bi.Mahita.
Ameongeza,”Tuweke jitihada katika kuwalea mapadri wetu kwani wamewaacha Baba, Mama na ndugu zao wanalitumikia Kanisa, hivyo padri akifiwa, kuuguliwa, akihitaji msaada wowote uwe wa usafiri... wewe kama WAWATA toa msaada haraka.”
Kwa upande wao, Katibu wa WAWATA Jimbo Kuu Songea na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi.Imelda Mbawala amesema katika Kongamano wanajifunza na kubadilishana uzoefu, mada mbalimbali huku wakiongozwa na kauli mbiu MWANAMKE MKATOLIKI MWENEZAJI WA HURUMA YA MUNGU, ambapo wamechagua viongozi wapya wa WAWATA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo Mwenyekiti ni, Bi. Rita Materu kutoka Jimbo Katoliki Iringa, Makamu Bi. Teresia Chilumba(Lindi), Katibu Bi.Imelda Mbawala(Songea), Katibu Msaidizi, Bi.Agness Hyera(Tunduru Masasi) na Mtunza hazina ni Bi.Rebeka Kapinga(Mbinga).
Naye, mlezi wa WAWATA, Sista Verena Kwimba amewaagiza masista kuwasaidia wanawake kufahamu kuwa kufunga siyo sala na sadaka tu bali pia na kusamehe yote,”tuwasaidie wanawake kama wanatoa sadaka na kusali wakati wa mfungo lakini wakitoka na manung’uniko mfungo wao unakuwa ni bure unafutwa.”
Mwenyekiti wa WAWATA Jimbo la Mbeya,Bi. Everada Mangwala amesema katika kongamano hilo wamefanya matendo ya huruma ya kuwatembelea watoto yatima katika kituo cha Igogwe na kuwapelekea mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula,seminari ndogo ya Mbalizi kituo cha Yatima Iyunga,walitembelea kituo cha malezi cha watawa wa kike.
Bi.Mangwala ametoa wito kwa wanawake kuanza kujiwekea akiba kidogo kidogo ili wapate kuwatolea wahitaji katika Kongamano la Kanda ya Kusini, mwezi Juni mwaka 2018 linalotarajiwa kufanyika jimboni Mbinga kwani kuhitimishwa kwa Kongamano la Mbeya ndiyo mwanzo wa maandalizi ya lile la Mbinga.
Katika ibada hiyo viongozi wastaafu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa WAWATA wa awamu iliyopita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jimbo Katoliki Mtwara, Bi. Verena Mahundi na Mweka hazina Bi. Agness Ng’owo wa Parokia ya Makambako, Jimbo Njombe kwa niaba ya viongozi wenzao wastaafu wameomba mshikamano uendelee kudumu huku wakifafanua zaidi kuwa WAWATA siyo kuvaa sare za vitenge tu bali ni mwanamke yeyote mkatoliki mbatizwa aliyefikisha umri wa miaka 18 kuusimamia na kuutekeleza kwa uadilifu utume wake kwa Kanisa.
No comments: