MASOMO YA MISA, JULAI 2, 2018
JUMATATU, JUMA LA 13 LA MWAKA

SOMO 1
Amo. 2:6 – 10, 13 – 16

Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Israeli, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu; nao hutwetea kuipotosha njia ya mwenye upole; na mtu na baba yake humwendea mwanamke mmoja, hata kulitia unajisi jina langu takatifu; nao hulijaza karibu na kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani, na katika nyumba ya Mungu wao hunywa divai ya watu waliotozwa fedha. Lakini nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni; lakini naliyaangamiza matunda yake toka juu, na mizizi yake toka chini. Pia naliwapandisha ninyi kutoka nchi ya Misri, nikawaongoza muda wa miaka arobaini jangwani, ili mpate kuimiliki nchi ya Mwamori.
Tazameni, nitawalemea ninyi, kama gari lilemeavyo lililojaa miganda. Naye apigaye mbio atapotewa na kimbilio; Wala aliye hodari hataongeza nguvu zake; Wala shujaa hatajiokoa nafsi yake; Wala apindaye upinde hatasimama; Wala aliye mwepesi wa miguu hataokoka; Wala apandaye farasi hatajiokoa nafsi yake; Naye mwenye moyo mkuu miongoni mwa mashujaa atakimbia uchi siku ile, asema Bwana.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 50:16 – 23 (K) 22

(K) Yafahamuni hayo, ninyi mnaomsahau Mungu.

Mtu asiye haki, Mungu amwambia,
Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)

Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye,
Ukashirikiana na wazinzi.
Umekiachia kinywa chako kinene mabaya,
Na ulimi wako watunga hila. (K)

Umekaa na kumsengenya ndugu yako,
Na mwana wa mama yako umemsingizia.
Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza;
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
Walakini nitakukemea;
Nitayapanga hayo mbele ya macho yako. (K)

Yafahamu hayo,
Ninyi mnaomsahau Mungu.
Nisije nikawararueni,
Asipatikane mwenye kuwaponya.
Atoaye dhabihu za kushukuru,
Ndiye anayenitukuza.
Naye autengenezaye mwenendo wake,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. (K)

SHANGILIO
Yn. 14:5

Aleluya, aleluya.
Bwana anasema: mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

INJILI
Mt. 8:18 – 22

Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.
Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.

Neno la Bwana... Sifa kwako ee Kristu.

No comments:

Powered by Blogger.