MASOMO YA MISA JUMAMOSI 7 APRILI 2018 OKTAVA YA PASAKA

SOMO 1:Md.4:13-21

Siku ile, makuhani na akida wa hekalu walipoona ujasiri wa Petro na Yohane, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Na wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu. Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao, wakisema, Tutawafanyieni watu hawa? Maana ni Dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana. Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohane wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia. Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 118:1, 14-21 (K) 21

(K) Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Au: Aleluya.

Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu,
Naye amekuwa wokovu wangu.
Sauti ya furaha na wokovu,
Imo hekaluni mwao wenye haki. (K)

Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.
Bwana ameniadhibu sana,
Lakini hakuniacha nife. (K)

Nifungulieni malango ya haki,
Nitaingia na kumshukuru Bwana.
Lango hili ni la Bwana,
Wenye haki ndio watakaoliingia.
Nitakushukuru kwa maana umenijibu,
Nawe umekuwa wokovu wangu. (K)

SHANGILIO
Zab. 118:24

Aleluya, aleluya.
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tutashangilia na kuifurahia.
Aleluya.

INJILI:Mk.16:9-15

Yesu alipofufuka alfajiri ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba. Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia. Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki. Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba. Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki.
Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, wakiwakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu. Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, makaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

No comments:

Powered by Blogger.