PATAKUFAHAMU MACHACHE KUHUSU SR.BERNADETA MBAWALA OSB:

MTAWA MZALENDO AMBAYE YUPO MBIONI KUTANGAZWA MWENYEHERI-MTAKATIFU.

Sr. Bernadeta ni nani?

Ni sista wa jamii ya Masista waafrika wa Mt. Agnes  Peramiho (Chipole), Tanzania.

Alizaliwa Peramiho mnamo tarehe 27 Oktoba 1911, akafariki 29 Novemba 1950.

Wazazi  wake Stefani na Agata walikuwa ni miongoni mwa Wakristu wa kwanza Peramiho. Katika ubatizo wake alipewa jina la Klara.

Alipokuwa mtoto aliingia shule ya misheni ya Peramiho na alipotimiza umri wa miaka 18 aliingia utawa akaitwa Sr. M (Maria) Bernadeta. Akaweka nadhiri zake za kwanza Novemba 11, 1934.

Sr.M Bernadeta alikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka 17 akayavumilia maumivu kwa ushujaa mkubwa.

Alijitahidi kujipatia ukamilifu na utakatifu pasipo kuchoka. Fadhila zilizojulikana kwake zilikuwa hasa upendo kwa Mungu na kwa jirani, utii, unyenyekevu, uvumulivu, ukweli na usafi mwangavu wa moyo.

Akajitoa sadaka kwa moyo mtakatifu wa Yesu kwa ajili ya Baba Mtakatifu, mapadre wa dunia nzima lakini pia Watawa wote Wabenediktini na wasio Wabenediktini.

Mnamo mwezi Juni mwaka 1949, mbali na ugonjwa wa Tumbo, aligundulika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu uliokuwa umefikia hatua mbaya sana.

Lakini hata hivyo, hakulegeza bidii ya kuvumilia mateso yote, bali alijibidiisha kuyasitiri huku akiwafurahisha masista wenzie kwa uchangamfu wake.

Tangu utoto wake, alimpenda sana Mama Bikira Maria kwa moyo wake mnyoofu. Wakati Fulani alipokuwa mtoto mwenye umri wa miaka miwili hivi, alishikwa na ugonjwa mkali wala haikutumainiwa kama atapona.

Hapo wazazi wake wema walimpeleka kanisani wakamtosa kabisa kwa Bikira Maria Imakulata,  na hatimaye akapona.

Muda wa miaka kadha kabla ya kifo chake alipata neema za pekee na majaliwa bora nayo yalimsaidia kuyastahimili mateso yake makali kwa ajili ya wongofu wa wakosefu na kwa wokovu wa watu walio katika hatari ya kufa.

Hapa Peramiho watu waliokuwa na shida kubwa walimlilia Sr. M. Bernadeta kwenye Kaburi lake kwa bidii na matumaini na wengi wao walisema kwamba walisaidiwa kwa maombezi yake.

Basi na tumuombe Mtumishi wa Mungu Sr. M. Bernadeta ili nasi tuweze kumtumikia Mungu kiaminifu.

Pia utakapojaliwa neema yeyote na Mungu mf. Kupona ugonjwa inabidi utoe taarifa ili kusaidia mchakato wa kumtangaza Sr. Bernadeta kuwa Mwenyeheri na baadae kuwa Mtakatifu.

Ikumbukwe kuwa Mwili wa Sr Bernadeta ulifukuliwa mnamo tarehe 24 Januari, 2012 mbele ya maaskofu wa Metropolitani ya Songea ambayo inahusisha majimbo  nane ambayo ni Songea, Njombe, Mbinga, Mbeya, Iringa,Tunduru Masasi,Lindi na Mtwara tayari kwa kuanza mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri na baadaye Mtakatifu.

Siku ya ufukuzi wa Kaburi hilo watu wengi walivutika kuja kuona kilichomo ndani, kwani lilikuwa ni jambo geni mno kwa wengi.

Lakini pili wengi walipatwa na shahuku ya kujua nini kinaweza kupatikana kwa mtu aliyekufa miaka hamsini(50) iliyopita.

NB: Kwa kipindi kirefu sasa, Kaburi lake limekuwa haliishiwi Watu wanaokwenda kuomba kwa ajili ya haja zao mbalimbali, na wengi wao wametoa ushuhuda wa kujibiwa maombi yao.

SOLI DEO HONOR ET GLORIA....

Ndani ya upendo wa Kristu,
Vicenza-Marie of the Eucharist.
Kwa hisani ya Fr. Herbert Meyer O.S.B (Catholic, Mission Liparamba, Mbinga-Songea E.A

1 comment:

  1. Ni kweli kabisa nimekuwa nikienda mara nyingi sana. Sehemu ile ni ya pekee kidogo kwangu na nina mshukuru mungu kwani amenipa nafasi kuona na kushuhudia utakatifu wake.

    ReplyDelete

Powered by Blogger.