MASOMO

SOMO 1:1Mak.2:15-29

Watumishi wa mfalme waliokuwa wakiwashurutisha watu kuasi wakaja Modini kuwalazimisha hata Matathia na wanawe walikuwapo. Watumishi wa mfalme wakamwambia Matathia, Wewe u kiongozi, mtu mkuu, maarufu katika mji huu. Una wana wako na ndugu zako wa kujiweka upande wako. Basi, tangulia wewe, uitimize amri ya mfalme, kama walivyofanya watu wote wa mataifa, na watu wa Uyahudi, nao waliosalia Yerusalemu. Ndipo wewe na wana wako watahesabiwa kati ya rafiki za mfalme; naam, wewe na wana wako watatuzwa fedha na dhahabu na vipawa vingi.
Matathia akajibu, akasema kwa sauti kuu, Hata mataifa yote katika milki ya mfalme wakimtii, wakiacha kila mtu dini ya wazee wake na kuchagua kuzifuata amri za mfalme, lakini mimi sivyo. Mimi na wanangu na ndugu zangu tutaishika njia ya agano la baba zetu. Isiwe kwetu kujitenga na sheria na maagano, hasha! Sisi hatutaisikiliza amri ya mfalme tugeuke katika dini yetu, kwa kuume wala kwa kushoto.
Alipokwisha kusema hayo, Myahudi mmoja alijitokeza machoni pa watu wote kusudi atoe dhabihu juu ya madhabahu iliyokuwapo Modini, kama ilivyoamriwa na mfalme. Matathia alipomwona, alishikwa na uharara, moyo wake ukatetemeka. Hasira yake ikatokeza hukumu, akamwendea mbio, akamwua pale madhabahuni. Kisha alimwua yule mtu wa mfalme naye, aliyekuwa akiishurutisha dhabihu, akaiangusha madhabahu. Hivyo alionyesha juhudi yake kwa sheria, kama juhudi ya Finehasi juu ya Zimri, mwana wa Salu.
Kisha, Matathia alipiga mbiu mjini kwa sauti kuu, akisema, Kila aliye na juhusi kwa ajili ya sheria na kutaka kulitetea agano, na anifuate! Naye na wana wake wakakimbilia milimani, wakiviacha vyote walivyokuwa navyo mjini.
Ndipo wengi waliokuwa wakitafuta haki na hukumu walikwenda jangwani wafanye maskani yao huko.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 50:1-2,5-6,14-15 (K) 23

(K) Nitawaonyesha wokovu wa Mungu.

Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
Toka maawio ya jua hata machweo yake.
Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri,
Mungu amemulika. (K)

Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru,
Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
Ukaniite siku ya mateso;
Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)

SHANGILIO
Yn. 14:5

Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

INJILI
Lk. 19:41-44

Yesu alipofika karibu ya Yerusalemu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo Amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

No comments:

Powered by Blogger.