MASOMO YA MISA JUMAMOSI TAREHE 18 NOVEMBA 2017 JUMA LA 32 LA MWAKA

SOMO 1:Hek.18:14-16,19:6-9

Mambo yote yalipokuwa kimya, na usiku ulikuwa katikati ya mwendo wake mwepesi, Neno lako Mwenyezi alishuka mbinguni kutoka kiti chako cha kifalme, shujaa aliye hodari, katika nchi iliyoposishwa hukumu, mwenye upanga mkali, ndio amri yako isiyopindika, akasimama na kujaza mambo yote mauti, na pindi alipogusa mbingu akaikanyaga nchi.
Kwa maana ulimwengu mzima, kwa kadiri ya asili yake, ulifanyika tena mpya, kwa kuzitii amri zako hizi na hizi, ili watoto wako walindwe wasipate dhara. Uwingu ulionekana uliokitia uvuli kituo chao, nan chi kavu ikapanda kutoka pale palipokuwapo maji kwanza, katika Bahari ya Shamu kukawa barabara isiyo na zuio, na uwanda wenye majani katika mawimbi yaumkayo. Hapo watu wako wakapita pamoja na majeshi yao yote, ambao kwa mkono wako walifunikwa, wakiisha kuona maajabu makuu. Wakazunguka-zunguka huru kama farasi, wakaruka-ruka kama wana-kondoo, wakikuhimidi Wewe, Bwana, uliyekuwa mkombozi wao.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 105:2-3, 36-37, 42, 43 (K) 5

(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.

Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. (K)

Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi.
Malimbuko ya nguvu zao.
Akawatoa hali wana fedha na dhahabu,
Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa. (K)

Maana alilikumbuka neno lake takatifu,
Na Ibrahimu, mtumishi wake.
Akawatoa watu wake kwa shangwe,
Na wateule wake kwa nyimbo za furaha. (K)

SHANGILIO
Zab. 119:105

Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.

INJILI:Lk.18:1-8

Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji Fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.
Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona Imani duniani?

No comments:

Powered by Blogger.