MIAKA 100 YA GOMBA LA SHERIA ZA KANISA
Baba Mtakatifu Pio X kunako tarehe 27 Mei 1917 katika Waraka wake wa Kitume“Providentissima Mater Ecclesia” alihidhinisha kwa mara ya kwanza Gombo la Sheria za Kanisa Katoliki kuchapishwa, kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Ni uamuzi uliotokana na changamoto mbali mbali zilizokuwa zinaoibuka katika shughuli za kichungaji na hivyo kuwepo umuhimu wa Sheria na kanuni ambazo zingesaidia kuratibisha huduma kwa watu wa Mungu. Sheria hizi zilipania kuwa ni msaada kwa familia ya Mungu katika ujumla wake. Papa Pio X katika maisha na utume wake, kama Padre na Askofu alikuwa amesheheni historia, utajiri na amana kubwa ya sheria za Kanisa. Alitamani kuona kwamba, mapadre katika maisha na utume wao, wanapata msaada wa kisheria ili kukabiliana na changamoto za shughuli za kichungaji.
Ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la XVI Kimataifa la Sheria za Kanisa, wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Gombo la Sheria za Kanisa lilipochapishwa kwa mara ya kwanza. Hizi ni sheria za Kanisa ambazo zimeboreshwa katika mfumo mpya, ili kuisaidia familia ya Mungu kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Mama Kanisa. Sheria za Kanisa na Katekisimu ya Kanisa Katoliki, zikawa ni vyombo vya muhimu sana kwa majiundo ya Kikristo na huo ukawa ni mwisho wa madaraka ya Mapapa katika masuala ya kiraia, ili kuliwezesha Kanisa kukita mizizi yake katika utume wa maisha ya kiroho.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kwamba, Gombo la Sheria za Kanisa limekuwa ni msaada mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika kipindi chote hiki cha karne moja, licha ya mapungufu na changamoto zake ambazo zinaweza kukubalika kuwa ni sehemu ya kazi ya mikono ya wanadamu. Wakati mwingine, Sheria hizi zimepindishwa katika nadharia na utekelezaji wake kwa vitendo, lakini hata hivyo, kwa ujumla Sheria za Kanisa zimekuwa na mwelekeo chanya kiasi cha kuliwezesha Kanisa kuvuka katika mawimbi mazito ya ulimwengu mamboleo, likiwa limeungana na kushikamana na watu wa Mungu, nguzo muhimu katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utume wa kimissionari, ambao umeliwezesha Kanisa kukita mizizi ya maisha na utume wake sehemu mbali mbali za dunia.
Gombo la Sheria za Kanisa limeliwezesha Kanisa kujikita katika maisha ya kiroho na kujimanua kutoka katika shughuli za kiraia, kwa kutekeleza ushauri wa Kiinjili kwa kumpatia Mungu kile kilicho cha Mungu na cha Kaisari, kile kilicho cha Kaisari. Kwa njia hii, Kanisa limeweza kujitegemea na kujiamini katika maisha na utume wake sanjari na kuchangia kuwa na mchakato makini wa walei katika masuala ya kidunia. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Gombo la Sheria za Kanisa ni wakati muafaka wa kuangalia leo na kesho ili kutambua na kuhimiza umuhimu wa kujikita katika Sheria ndani ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, hili ni Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, mahali ambapo Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa zinapewa umuhimu wa kwanza, kwa kusaidiwa na Sheria za Kanisa. Ni wakati muafaka wa kutafakari juu ya umuhimu wa majiundo ya kisheria ndani ya Kanisa, kwa kujikita katika mikakati ya kichungaji mintarafu Sheria za Kanisa na kama mwongozo kwa ajili ya afya ya roho za waamini “Salus animarum” pamoja na kuhakikisha kwamba, haki inatendeka katika Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujifunza ili hatimaye, waweze kuzifahamu Sheria za Kanisa na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa, kama kielelezo makini cha upendo kwa Kanisa! Jamii pasi na sheria hapo hakuna haki “Nulla est charitas sine iustitia”. Huu ni mkazo ulitolewa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Barua yake kwa Waseminari baada ya kuadhimisha Mwaka wa Mapadre Duniani, 2010. Naye Mtakatifu Yohane Paulo II katika uzinduzi wa Gombo Jipya la Sheria za Kanisa kunako mwaka 1983 alikazia umuhimu wa Mama Kanisa kuendelea kutafsiri lugha ya Sheria za Kanisa kadiri ya ufahamu wa Kanisa kama ulivyofafanuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Lengo anasema Baba Mtakatifu Francisko, ni kuliwezesha pia Kanisa kumwilisha katika maisha na utume wake wa kila siku kwa watu wa Mungu, Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hapa kwa mfano ni Barua Binafsi, “Motu proprio” inayorekebisha na kurahisisha utenguaji wa ndoa za Kikristo. Kumbe, Gombo la Sheria za Kanisa ni chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa vizazi baada ya vizazi.
Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee: “Urika wa Maaskofu” na “Dhana ya Sinodi” katika uongozi kuanzia ndani ya Makanisa mahalia sanjari na uwajibikaji makini wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Mambo mengine ni Uekumene na Huruma kama mihimili mikuu ya kichungaji; uhuru wa kidini wa mtu binafsi, watu wote na taasisi katika ujumla wake. Waamini walei walio wazi na wenye mwelekeo chanya; ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali hata katika utofauti wake ni kati ya mambo msingi yanayoweza kutekelezwa kwa dhati na Sheria za Kanisa kama chombo cha majiundo, ili kuwasaidia Wakristo kukua na kukomaa na kujisikia kuwa ni sehemu ya utamaduni unaojibu kwa dhati kabisa mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
No comments: