JIFUNZE VITU MUHIMU KATIKA MISA TAKATIFU

Watu wengi hawaelewi sawa sawa ukuu na utajiri wa Ibada ya Misa Takatifu, hivyo hawashiriki sawa sawa, na matokeo yake hawapati ukombozi unaopatikana au unaokusudiwa. Kila kipindi kina maana kubwa.
 Ni vizuri kuwa na maandalizi  mazuri kwa ajili ya Misa. Wengine wanakuja kumalizia uchovu kanisani, huanza kusinzia wakati wa kusikiliza neno hadi mahubiri, yaani kila ikitokea utulivu kasinzia.
Wengine hutumia wasaa wa Misa kusali Rosali, nadhani muumini ambaye ana mapendo ya kweli kwa Sala ya Rosali ni vyema  akajipangia muda muafaka wa kuisali ili apate Neema, maana kwa kusali Rosali wakati wa Misa anakuwa amekosa yote, yaani Neema ya Misa kwa vile hajashiriki na ya Rosali ataikosa kwa kuwa hakuisali katika muda muafaka.
 Na wengine hatufahamu kuwa Makuhani wana mavazi maalum ya kutolea sadaka ya Misa, rangi ya vazi hufafanua ujumbe wa wakati au Misa husika. Tuliliongelea hili siku moja humu, Zambarau ni rangi ya toba na matumaini, hutumika wakati wa Majilio na Kwaresima, halafu katika Misa ya Toba na ya wafu.
Nyeupe ni rangi ya utakatifu, huvaliwa kipindi cha Noeli na Pasaka, pia katika Misa ya Ubatizo, Watakatifu wasio wafia dini, Sikukuu ya Ekaristi au Komunyo ya kwanza.
Nyekundu ni alama ya Damu na Roho Mtakatifu, huvaliwa sikukuu ya Matawi na ijumaa kuu, pia Pentekoste na Kipaimara, pia Watakatifu wafia dini.
Kijani kibichi ni alama ya ustawi na mavuno, huvaliwa kipindi cha kawaida kisicho na adhimisho maalum, ni kipindi cha kutumiwa Neema tulizozipokea.
Wengine tunaona tu Chetezo na Ubani hatuelewi chochote, Tangu Agano la kale, ubani ni moja ya vitu muhimu kwa sadaka kwa Mungu, Mamajusi wa mashariki walipokuja kumwona Yesu, moja ya zawadi walizomletea ilikuwa ni Ubani, wakimaanisha kuwa Yesu ni Mungu, kwani ni Mungu pekee anayepewa au kupuliziwa Ubani. Katika Agano jipya, mambo ya Ubani yanatajwa pia katika Ibada za mbinguni katika kitabu cha ufunuo. Wakati wa Misa kila kitu kinachomwakilisha Mungu hufukiziwa Ubani, kama vile Madhabahu, Ekaristi, Msalaba, Mshumaa wa Pasaka, na kadhalika. Roho Mtakatifu aliye ndani ya kila Mwamini hufukiziwa Ubani. Pale tunapoelekezewa sisi hatufukiziwi sisi kama sisi bali Mungu aliye ndani yetu.
 Wengine pia tunaona tu mshumaa au taa katika Tabenaklo bila kufahamu, taa au mshumaa unaowaka inadhihirisha uwepo wa daima wa Kristo katika Ekaristi, mishumaa hutumika kila wakati wa Misa kuwakilisha uwepo wa Kristo aliye nuru ya ulimwengu.
 Sisi wengine pia huwa tunaona tu Kwaya ipo pale inaimba, kumuimbia vizuri Mungu ni kusali mara mbili, kikundi cha Kwaya ni Kiongozi wa nyimbo za Ibada, sote tunapaswa na tunalazimika kuimba hasa pale zinapoimbwa nyimbo tunazozijua, ndio maana ya kushiriki katika Misa na sio kuhudhuria tu.
Kwaya husaidia kukoleza na kuhamasisha uzuri wa Ibada yetu katika kutufanya hai, tangu Ibada za Agano la kale tunapata wanakwaya, pia inatupasa kuiga mfano wa mfalme Daud pale alipomwimbia Mungu zaburi, nyimbo nyingi za kanisani zinatoka katika zaburi haswa za katikati ya Masomo, kwa kuimba zaburi tunamsifu na kumshukuru Mungu Muumba wetu kwa Yale anayotujalia katika maisha yetu.
Hongereni wanakwaya kama wapo humu ndani.
 Huwa tunaona tu maandamano ya Padre na watumishi kutoka Sakristia, Maandamano ya Padre na watumishi kutoka Sakristia kuja kanisani na hatimaye Altareni kutoa sadaka ndiyo tukio la Yesu kuingia Yerusalemu kwa shangwe na hatimaye Kalvari kwa ajili ya kufa sadaka yetu, lakini Ibada ya Misa haiishii tu na kifo cha Bwana msalabani, Bali pia ufufuko wake na kupaa kwake mbinguni kwa utukufu.
 Mwanzo wa Ibada, tunafahamu kuwa, "Wanapokusanyika pamoja wawili au watatu kwa jina langu, Mimi nipo katikati yao."(Mt 18:20) Kitendo cha kuwa na kusanyiko tu kwa ajili ya Bwana tayari yeye anajiunga nasi, Padre anaanza kwa kutujulisha kuwa tumekusanyika hapa "kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu" na sisi tunajibu "Amina" tukiwa na maana ya kwamba ni hakika ndiyo lengo letu kuwepo hapa, pamoja na maana hiyo, hapa tunajibariki kwa ishara ya Msalaba tunajichora na kwa maneno tunayotamka, yaani baraka ya Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama tujuavyo, Msalaba ndiyo chemchemi ya baraka na Neema zote tunazoweza kupokea kwa Bwana.
Kisha tunamwomba Bwana ajiunge nasi, yaani atimize ahadi yake ya kuwa pamoja nasi,
Ndiyo Padre anatuambia sasa, "Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote". Nasi tunajibu kwa kumtamkia mwadhimisha Ibada uwepo wa Bwana Yesu mwenyewe ndani yake katika kutekeleza huduma yake.
 Yesu alipoanza kazi yake ya ukombozi alisema,"Tubuni na kuiamini Injili" (MK1:15) akimaanisha kuwa hicho ndicho kitu cha kwanza cha msingi kwa sababu tuko wadhambi mbele za Mungu aliye Mtakatifu sana. Na kutubu na kuiamini injili vinaenda kwa pamoja na tena vinategemeana sana. Huwezi kuiamini injili kama hauko tayari kutubu, na hauwezi kutubu kama hauko tayari kuiamini Injili. Tunapotubu tunajistahirisha utimilifu wa msamaha wa dhambi katika sadaka ya msalabani tunayoielekea katika Ibada.
Kwa hiyo katika hatua hii ya mwanzo huwa tunajipatanisha kwanza na Mungu na jirani zetu kabla ya kumtolea Mungu sadaka yetu. "Nakuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu."
Ni lazima kuwa na Moyo wa Toba kwa Mungu na jirani kwani tumekuja kutoa sadaka ya upatanisho. Ili maungamo yetu yalete maana ni vema kuja kwa Misa ukiwa umepatana na watu wote mliokosana.

4 comments:

  1. Nimuongozo mzuri ambao waumini wengi wetu hatujui matukio mbalimbali wakati wa adhimisho la misa takatifu.

    ReplyDelete
  2. Kweli nimeona ni vyema kukumbushana mambo muhimu katika misa takatifu ambayo wengi wetu tunakuwa hatuyaelewi.

    ReplyDelete

Powered by Blogger.